Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amezitaka taasisi zenye miundombinu ndani ya hifadhi ya barabara ya Kibena-Lupembe-Mfuji/Taweta (Morogoro/Njombe) kushirikiana na Wakala wa Barabara (TANROAD) kufanya tathmini ya gharama za kuhamisha miundombinu yao ili kuepusha ucheleweshaji wa mradi huo wa kilomita 126.17 kwa kiwango cha lami.
Mtaka alitoa agizo hilo jana tarehe 25 Februari 2025 wakati wa kikao maalum ofisini kwake, ambacho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Edwin Swalle, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omari, na Meneja wa TANROAD Mkoa wa Njombe, Injinia Ruth Shalua. Alisisitiza kuwa taasisi zote husika zinapaswa kushiriki mapema katika mchakato huo ili kuepusha changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi.
“Lazima TANESCO, mamlaka za maji na TTCL washirikiane na TANROAD kufanya tathmini mapema. Kila taasisi ijue miundombinu yake inavyoathirika ili isisubiri hadi mkandarasi aingie site ndipo waanze kutatua changamoto. Tusiruhusu mradi huu kusimama kwa sababu ya kuchelewa kuhamisha nguzo au mabomba,” alisema Mtaka.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROAD Mkoa wa Njombe, Injinia Ruth Shalua, alieleza kuwa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo ilitangazwa Februari 12 na inatarajiwa kufunguliwa Machi 26, huku wakandarasi wakipewa nafasi ya kutembelea eneo la mradi kuona vyanzo vya malighafi za ujenzi.
Mtaka alihitimisha kwa kuwataka wadau wote kuhakikisha michakato ya awali inakamilika kwa wakati ili mradi huo muhimu kwa uchumi wa Njombe na Morogoro usikwame.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.