Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ameahidi ushirikiano thabiti kati ya serikali ya mkoa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ili kuimarisha sekta ya kilimo na biashara ya mazao, hususan parachichi. Akizungumza baada ya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola, Mhe. Mtaka alisisitiza kuwa Njombe imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa parachichi, hivyo serikali ya mkoa itahakikisha mafanikio hayo yanalindwa na kuendelezwa.
Kwa upande wake, Bi. Mlola alieleza kuwa COPRA, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) pamoja na Umoja wa Wakulima wa Parachichi (ASTA), inaendelea kutathmini changamoto zinazokumba uzalishaji na biashara ya parachichi katika maeneo yanayozalisha zao hilo nchini. Kikosi kazi maalumu kimeundwa ili kuchambua na kutatua changamoto hizo kwa lengo la kuboresha zaidi sekta hiyo. Parachichi ni zao muhimu kwa uchumi wa Njombe, likichangia pato la wakulima na mapato ya mkoa kupitia mauzo ya ndani na nje ya nchi.
Katika kuhakikisha zao la parachichi linakuwa na thamani zaidi, Njombe tayari imeshatatua changamoto ya uongezaji thamani kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata mafuta ya parachichi chini ya Kampuni ya Avoafrica. Kiwanda hicho, ambacho tayari kimeanza uzalishaji, kinatoa fursa kwa wakulima kuuza mazao yao kwa uhakika na kwa bei nzuri, hivyo kuongeza kipato cha wakulima na kukuza uchumi wa mkoa kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.