NAIBU Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amesema ifikapo mwezi Novemba mwaka huu kilomita 36 za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Njombe hadi Moronga yenye urefu wa kilomita 53.9 zitakuwa zimekamilika ikiwa ni moja ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo kwa kiwango cha lami,kati ya kilomita 110 za kutoka Njombe hadi wilayani Makete.
Akiwa Mkoani hapa Mh.Kwandikwa ameanza ziara ya siku tatu ya kutembelea miradi ya ujenzi wa barabara na kujionea kasi ya ujenzi wa kipande cha barabara ya Njombe hadi Moronga yenye urefu wa kilomita 53.9 inayojengwa kwa gharama` ya shilingi bilioni 107 mkoani hapa,ambapo amemtaka mkandarasi wa kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) ya nchini China kuharakisha kukamilisha barabara hiyo kwa kuwa wananchi wanataka kuona barabara.
“Tunatarajia kilomita 36 zitakamilika ifikapo mwezi Novemba, hivyo nawaagiza ongezeni kasi ya ujenzi usiku na mchana kipindi hiki ambacho mvua kidogo zimesimama,ili niwahakikishie wananchi kwa ujumla wake na wilaya zetu za Makete na Wanging’ombe kwamba nia ya serikali ni kuona wananchi wanapata barabara,” alisema.
Naibu waziri ameongeza kusema kuwa kwa sasa wananchi hawahitaji maneno ya kitaalam bali muhimu kutoka kwao ni kuona barabara inakamilika ili waweze kusafirisha mazao yao kwa wakati kwenda sokoni.
Naye Meneja wa Tanroads Mkoa wa Njombe, Yusuf Mazana awali alimweleza Naibu Waziri wa Ujenzi kuwa kutokana na mkandarasi kuongeza rasilimali watu hasa wataalamu wa vitengo mbalimbali, hivi sasa kasi ya ujenzi wa barabara ya Njombe hadi Makete imeendelea kuongezeka.
“Ujenzi kwa sasa umefikia asilimia 34.6 na kazi kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa pande zote mbili inatarajia kukamilika tarehe 2 Januari, 2020,” alisema Mazana.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa mradi huo Lusekelo Kijalo alimuahidi Naibu Waziri Kwandikwa kuwa hadi kufikia mwezi Novemba, kilomita 36 zitakuwa zimekamilika kwa kiwango cha lami jambo ambalo litatoa matumaini kwa wakazi wa Njombe.
Nae Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe mkoani hapa komredi Ali Kasinge alisema serikali imeendelea kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyofanywa na wananchi wasiokuwa waaminifu kwenye ujenzi wa mradi huo na kwamba jeshi la polisi limejipanga kukomesha tabia za wizi wa mafuta na vifaa mbalimbali vya ujenzi kwenye mradi huo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Moronga wakizungumza kwa nyakati tofauti waliipongeza serikali kwa hatua yake ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kueleza namna itakavyowasaidia kusafirisha mazao ya mbao na viazi mviringo ambavyo katika maeneo hayo yamekuwa yakilimwa kwa wingi.
“Tunaridhika na kasi ya ujenzi kwa sasa tunaona mambo yanaenda vizuri,kwa kweli huko nyuma hali ya barabara ilikuwa mbaya, tulikuwa tunashindwa kusafirisha mazao yetu lakini ikikamilika barabara hii itatukomboa sana,”alisema Asifiwe Kiyombo.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.