Njombe, 28 Aprili 2025
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ndugu Peter Ilomo, ameanza ziara rasmi ya kikazi katika Mkoa wa Njombe leo tarehe 28 Aprili 2025, ambapo anatarajiwa kuhitimisha ziara hiyo tarehe 05 Mei 2025.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) katika ngazi za Halmashauri, Kata na Vijiji, ili kuhakikisha kuwa miradi ya TASAF inatekelezwa kwa ufanisi na kuwafikia walengwa waliokusudiwa.
Mara baada ya kuwasili mkoani hapa, Ndugu Peter Ilomo alipokelewa na Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu, Ndugu Joseph Mutashubilwa akimuwakilisha Katibu tawala wa Mkoa wa Njombe.
Akizungumza wakati wa mapokezi, Ndugu Mutashubilwa alimpongeza Mwenyekiti Ilomo kwa uamuzi wa kufanya ziara hiyo muhimu, akieleza kuwa Mkoa wa Njombe umejipanga kikamilifu kushirikiana nae kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unafikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake, Ndugu Peter Ilomo alieleza kuwa ziara hiyo inalenga kujionea kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo, kusikiliza changamoto kutoka kwa walengwa, pamoja na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa TASAF katika maeneo yote atakayoyatembelea.
Katika siku za usoni, Mwenyekiti huyo atafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Njombe, akikutana na wanufaika wa mpango huo pamoja na viongozi wa serikali za mitaa, huku akisisitiza usimamizi madhubuti wa miradi ya TASAF kwa manufaa ya wananchi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.