Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amefanya mazungumzo ya kina na Mkurugenzi wa kampuni ya Kanji Lalji Limited, Bw. Aly Sultan Kanji Lalji, katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo jijini Mbeya. Mazungumzo hayo yalilenga kuhamasisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya kilimo mkoani Njombe, hususan kilimo cha kahawa.
Katika kikao hicho, Mhe. Mtaka alimkaribisha rasmi Bw. Aly Kanji kuwekeza mkoani Njombe, akieleza kuwa mkoa huo una fursa kubwa katika uzalishaji wa kahawa kutokana na ardhi yake yenye rutuba, hali ya hewa nzuri na nguvu kazi ya kutosha. Alieleza kuwa serikali ya mkoa imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na iko tayari kutoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha uwekezaji wa sekta binafsi, hasa kwenye kilimo chenye tija na soko la uhakika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanji Lalji Ltd., Bw. Aly Kanji, alieleza kufurahishwa na wito huo wa uwekezaji na kuahidi kuwa kampuni yake iko tayari kuangalia kwa dhati uwezekano wa kuanzisha miradi ya kilimo cha kahawa mkoani Njombe. Alisema Kanji Lalji, ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 100 katika sekta ya usafirishaji na kilimo, inatambua thamani ya ardhi ya Njombe na inalenga kutumia utaalamu wake kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wa ndani.
Mhe. Mtaka alihitimisha kwa kusema: “Mkoa wa Njombe umejipanga kuwapa wawekezaji wote ushirikiano wa karibu. Ardhi yetu ni ya rutuba, mazingira ni mazuri, na serikali iko tayari kuwezesha kila hatua ya uwekezaji. Tunawakaribisha wawekezaji kama Kanji Lalji kuja kushirikiana nasi kukuza uchumi wa wananchi wetu kupitia kilimo cha kisasa.”
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.