Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Njombe Bi Kuruthum Sadick kuwasimamisha kazi watumishi sita wa kituo cha afya cha mjini hapo baada ya kubainika upotevu wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 15.
Agizo hilo lilitolewa wakati wa ziara ya mwendelezo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kushughulikia matukio ya wizi yanayotokea katika hospitali na vituo vya afya mkoani hapa.
“Mkurugenzi uchukue hatua hapa simamisha na hatua za haraka za kinidhamu zifanyike kwa kufuata taratibu zote na Mkuu wa kituo cha Polisi tukitoka hapa beba hawa watu wote nenda nao wakatoe maelezo,wakitoa maelezo hatua za kinidhamu za kiutumishi na uchunguzi ufanyike,”alisema Mtaka.
Awali akisoma taarifa ya upotevu, Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Njombe Dk. Jabil Juma alisema vifaa tiba vilivyoibiwa ni kipimo cha wingi wa damu,mashine ya kupima mkojo,vitepe kwa ajili ya kupima Ukimwi.
“Mshine moja ya uchunguzi wa mkojo haikuonekana stoo ilipokelewa Januari 2022, lakini pia tulibaini mashine moja ya uchunguzi wa wingi wa damu pia haikuwepo maabara,”alisema Juma.
Watuhumiwa wa upotevu huo akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Maabara,Izack Kayombo alisema mashine ya kupima wingi wa damu waliiazimisha katika kituo cha afya Lupembe halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Hata hivyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Dk.Juma Mfanga alisema katika ufuatiliaji wake taarifa hizo vifaa hivyo havipo maeneo yanapoelezwa vimepelekwa.
“Kwenye ufuatiliaji ambao tumeufanya imeonekana kwamba mashine ya kupima mkojo ndio ilienda kituo cha afya Lupembe kwa sababu tunasimamia vituo vyote vya afya kwenye mkoa wao wanakiri hawajapokea,inamaana kuna mahali hapa katikati viliishia,”alisema Mfanga.
Wakati huo huo,Mkuu wa Mkoa alisema inasikitisha kuona kwamba inafika mahala unakuwa na watumishi ambao unawaajiri alafu wanaiba.
‘’Kwanza nikuombe Mganga Mkuu wa Mkoa kufanyike ukaguzi vituo vyote vya afya vya mkoa wa Njombe,ukaguzi ufanyike hospitali zote za wilaya mkoa wa Njombe tuangalie vifaa tulivyopokea,utokaji wake,vilivyopo na ambavyo vimetumika hiyo taarifa tuwe nayo kwa sababu tusije tukawa na vifaa alafu tuna madalali kwenye ofisi za umma,’’alisema Mtaka.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe,Kamishna msaidizi Mahmoud Banga alisema hadi sasa watu 10 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma za wizi katika kituo cha afya Njombe mjini na hospitali ya rufaa mkoa wa Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.