Mwekezaji kutoka Kampuni ya Ovolio Industries Ltd nchini Uganda ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, ambapo alipokelewa na Mhe. Anthony Mtaka kwa mazungumzo ya uwekezaji. Timu hiyo ya wawekezaji imeongozwa na mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Kampuni hiyo, Ndg. Omar Ababneh.
Katika mazungumzo yao, mwekezaji huyo alieleza dhamira yao ya kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mafuta ya parachichi mkoani Njombe, wakitarajia kutumia eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho. Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya zao la parachichi na kuwainua wakulima wa zao hilo katika mkoa wa Njombe.
Akizungumza baada ya kupokea wageni hao, Mhe. Anthony Mtaka alisema Serikali ya Mkoa wa Njombe itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia njema na maendeleo ya mkoa. “Tunawakaribisha kwa mikono miwili. Uwekezaji katika kiwanda hiki utasaidia kuongeza thamani ya parachichi, kuongeza ajira na kuongeza kipato cha wakulima wetu,” alisema Mhe. Mtaka. Aliahidi kuwa mkoa uko tayari kusaidia upatikanaji wa eneo stahiki kwa ajili ya mradi huo wa kimkakati.
Ujio wa mwekezaji huyu unaongeza hamasa kwa juhudi za Mkoa wa Njombe katika kukuza sekta ya viwanda na kuunga mkono jitihada za kitaifa za kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.