Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amekutana na wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Njombe (NJOSS), kwa lengo la kuwapa hamasa na kuwatakia kila la heri katika mtihani wao wa taifa unaotarajiwa kuanza Mei 5 mwaka huu. Katika mkutano huo, Mhe. Mtaka amesema serikali ya mkoa inaamini katika uwezo wa wanafunzi wake na inatarajia matokeo bora yatakayotangaza heshima ya Njombe kitaifa.
Mhe. Mtaka amewaasa wanafunzi hao kwenda kwenye mitihani hiyo wakiwa na nidhamu, utulivu na kujiamini, akisisitiza kuwa maandalizi yao yamekuwa ya kina na yanaonesha matumaini makubwa ya mafanikio. “Najua mmejiandaa, mmefunzwa, na mmepambwa na maadili. Ni wakati wenu sasa kuwasha taa ya ushindi. Njombe ni mkoa wa matokeo makubwa,” alisema kwa msisitizo.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo kuwaasa wanafunzi kote Njombe kuchukulia mtihani huo kama daraja la kuelekea mafanikio makubwa, huku akisisitiza kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kujenga taifa. “Fanyeni mitihani hii kwa bidii na uadilifu, mkijua kuwa kila jasho lenu ni mbegu ya kesho yenu. Tunawaombea mtihani mwema na mafanikio makubwa.”
Katika kuhitimisha, Mhe. Mtaka alieleza kuwa Mkoa wa Njombe una mazingira rafiki ya kielimu na walimu mahiri walioweka msingi imara kwa wanafunzi, hivyo anaamini mkoa huo utakuwa miongoni mwa mikoa itakayofanya vizuri zaidi kitaifa. “Tutangaze ushindi kupitia akili zenu. Hili ni taifa lenu, na sasa ni zamu yenu kulijenga kwa maarifa.” alisema.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.