Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa idara Mkoani Njombe kuwa wabunifu kwa ajili ya kuwaletea wananchi Maendeleo.
Amesema hayo akiwa kwenye Baraza la maalumu la Madiwani tarehe 15 Julai 2023 Halmashauri ya Wilaya ya Makete wakati wa kujadili hoja za Mkaguzi zilizoibuliwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Mhe. Mtaka amesema ubunifu wa miradi ya Maendeleo ndio chachu ya ukuaji wa uchumi kwa Maendeleo ya Taifa, Wilaya, Kata, Vijiji na hatimaye mwananchi mmoja mmoja jambo ambalo litaifanya Serikali kuonekana inatekeleza wajibu wake wa kuwaletea wananchi maendeleo.
“Dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi wake Maendeleo inawapaswa Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Idara kama wasaidizi wake wamsaidie na wasilaze akili lazima tuwe wabunifu”
“Kuwaza maendeleo sio dhambi bali lazima uwezo wetu wa kufikiri uongezeke, lakini nampongezaMkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe kwa ubunifu ambao anaufanya Makete kwa kuibua miradi ambayo inaweza kuwaingizia kipato kikubwa na kuongeza pato la Halmashauri”.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe amesema Halmashauri inamikakati mbalimbali ya kuibua miradi mipya ambapo kwa sasa imeibua mradi mkubwa wa Stendi ya Mabasi Kimani iliyopo Kata ya Mfumbi.
Makufwe ameongeza kuwa Halmashauri inataka kuwa na miradi yenye tija na kuongeza mapato badala ya hali ilivyo sasa kutegemea mapato kutoka kwenye vyanzo vilivyozoeleka vya Zao la Viazi na Mbao.
Jacrene Mrosso Afisa Maendeleo Halmashauri ya Wilaya ya Makete amesema kupitia mikopo ya 10% ambayo inatolewa na Halmashauri, wamekopesha fedha kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakijishughulisha na Kilimo cha ngano, Viazi, Ufugaji, Ujasiriamali na Bodaboda ili kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.