Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, pamoja na Menejimenti yote kwa ujumla, inaungana na Watanzania wote katika kuadhimisha kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere. Mwalimu Nyerere, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, ni kielelezo cha uongozi wa busara, utu, usawa, na haki. Leo, tunamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kujenga misingi imara ya taifa huru na lenye umoja.
Katika maadhimisho haya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe imeeleza kuwa Nyerere aliwaweka wananchi katikati ya kila jitihada za maendeleo ya taifa. Uongozi wake ulizingatia umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika maamuzi na michakato ya maendeleo. Kupitia sera zake za Ujamaa na Kujitegemea, alihamasisha jamii kufanya kazi kwa bidii, kwa pamoja, ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata nafasi sawa ya kushiriki katika ustawi wa taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe tunaamini kwamba Mwalimu Nyerere alianzisha tunu za Umoja na Amani ambazo zimekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya Tanzania hadi sasa. Amani aliyoijenga imewezesha taifa letu kuendelea katika mazingira ya utulivu, huku Umoja ukiendelea kuwa chachu ya mafanikio katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kijamii, na kisiasa.
Kwa kuhitimisha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe tunawaeleza wananjombe na watanzania kwa ujumla kuwa, tunaendelea kuenzi na kudumisha maono ya Mwalimu Nyerere. Katika kumbukizi hii, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Athony Mtaka anawamehimiza wananchi wote wa Mkoa wa Njombe kuendelea kushikamana na kutetea tunu hizi, ili kizazi cha sasa na kijacho kiendelee kufurahia matunda ya uhuru, maendeleo, na amani aliyoyapigania kwa dhati.
Mhe. Mtaka pia ameongeza, "Kama alivyosisitiza Mwalimu, Serikali za Mitaa ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa. Ni wakati wa wananchi kuonyesha uzalendo wao kwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ili kuhakikisha tunapata viongozi wenye maono na uwezo wa kusimamia maslahi ya jamii. Tunapoelekea uchaguzi huu, ninawahamasisha wananchi wote wa Njombe kujiandikisha mapema na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huu wa kihistoria, ili tuendelee kujenga jamii yenye usawa, haki, na maendeleo."
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.