Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa,tarehe 25 Septemba 2024 ameongoza kikao cha BBT kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe. Kikao hicho kimehudhuriwa na kundi kubwa la vijana na wanawake kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Njombe, kwa lengo la kujadili mikakati ya maendeleo na fursa za kiuchumi haswa kwenye sekta ya Kilimo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Gwakisa alisisitiza umuhimu wa vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla. Alieleza kuwa kundi hili lina nafasi kubwa katika kufanikisha mipango ya maendeleo na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
"Vijana ni nguzo muhimu katika kujenga taifa. Ninawaomba mjitokeze na kuchangamkia fursa zilizopo, zikiwemo za kilimo, Pia wanawake, nafasi yenu ni kubwa katika kuleta mabadiliko, siyo tu ndani ya familia bali pia katika jamii nzima," alisema Mhe. Gwakisa.
Aidha, Mhe. Gwakisa alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa vijana kuwa wavumilivu, wabunifu, na kuchukua hatua za makusudi katika kujenga maisha bora. Aliwasihi vijana kuacha tabia ya kukata tamaa na badala yake wawe na mtazamo chanya kuhusu mustakabali wa maisha yao.
"Pambaneni kwa bidii na msiruhusu changamoto kuwa vikwazo. Dunia inabadilika kwa kasi, na ni muhimu sana kutumia teknolojia na ubunifu katika kutatua matatizo ya kila siku. Serikali ipo pamoja nanyi katika kuhakikisha mnapata mazingira bora ya kufanikisha ndoto zenu," aliongeza.
Mhe. Gwakisa aliwahakikishia vijana na wanawake kuwa serikali ya wilaya itaendelea kuwaunga mkono na kuwekeza katika miradi itakayosaidia kuinua hali zao za kiuchumi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.