Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, leo amekuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa huduma mpya za uchunguzi na matibabu ya mfumo wa chakula (Endoscopy Services) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watoa huduma za afya, pamoja na wananchi wa Njombe waliojitokeza kushuhudia tukio hili muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya katika mkoa huo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mtaka ameipongeza hospitali hiyo kwa hatua kubwa ya kuboresha huduma za matibabu, akieleza kuwa huduma za endoscopy zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya ya wananchi kwa kuwapatia uchunguzi wa mapema na matibabu sahihi kwa magonjwa ya mfumo wa chakula.
"Huduma hii mpya ya endoscopy itawasaidia wananchi wetu kupata uchunguzi wa mapema wa magonjwa ya mfumo wa chakula kama vidonda vya tumbo, saratani na matatizo mengine bila kulazimika kusafiri kwenda nje ya mkoa. Hii ni hatua kubwa ya kuboresha sekta ya afya katika mkoa wetu," alisema Mhe. Mtaka.
Aidha, alieleza kuwa uwekezaji katika huduma za afya ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha huduma za matibabu zinaboreshwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi vijijini na mijini.
Huduma hizi mpya zinatarajiwa kupunguza idadi ya wagonjwa wanaohitaji kusafiri kwenda mikoa mingine au nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yanayohusisha mfumo wa chakula. Pia, zitatoa nafasi kwa wataalamu wa afya katika hospitali mkoa wa Njombe kutoa matibabu kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Mtaka alitoa wito kwa wananchi wa Njombe kufika hospitalini kupata huduma za uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuepuka matatizo makubwa yanayoweza kuzuilika endapo yatatibiwa mapema.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.