Njombe, Tanzania – Katika kuimarisha usimamizi wa taarifa za watumishi wa umma, Maafisa wa Kada ya Utumishi kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Njombe wamepatiwa mafunzo maalum yanayolenga kuongeza uelewa na ufanisi katika matumizi ya mifumo ya Serikali za Mitaa.
Mafunzo hayo yameenda sambamba na zoezi la kitaifa la usafishaji wa taarifa za kiutumishi (data cleaning) kupitia mfumo wa e-Watumishi, ambapo yanatarajiwa kufanyika kwa siku saba mfululizo kuanzia leo Aprili 22, 2025. Zoezi hilo linasimamiwa na Maafisa Waandamizi kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, likiwa na lengo la kuhakikisha taarifa zote muhimu za watumishi zinahakikiwa, kurekebishwa na kuwasilishwa kwa usahihi na kwa wakati.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, yakiratibiwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Utawala, Bw. Lewis Mnyambwa. Akizungumza na washiriki, Bw. Mnyambwa alisisitiza umuhimu wa usahihi, uwajibikaji na uadilifu katika utunzaji wa taarifa za kiutumishi.
“Ni wajibu wa kila Afisa Utumishi kuhakikisha taarifa zote za watumishi zinasafishwa, kuhakikiwa na kuwasilishwa kwa wakati,” alisema Bw. Mnyambwa, akirejea Waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Na. 1 wa mwaka 2010 unaosisitiza usimamizi madhubuti wa rasilimali watu serikalini.
Zoezi la usafishaji linahusisha uhakiki wa taarifa muhimu za watumishi kama majina, tarehe za kuzaliwa, taarifa za ajira, vituo vya kazi, viwango vya elimu, pamoja na kuambatisha nyaraka muhimu katika mfumo wa e-Watumishi.
Aidha, watumishi walioko kwenye orodha ya malipo (Payroll) lakini hawapo kazini tangu Julai 1, 2022, wanapaswa kubainishwa na sababu za kutokuwepo kwao kufafanuliwa, ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma.
Serikali inaamini kuwa kupitia hatua hii, msingi wa utawala bora, uwajibikaji na tija kazini utaimarika kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.