Njombe, Juni 3, 2025 – Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, ameongoza kikao cha maandalizi ya Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yatakayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, yakihusisha wakulima kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Kikao hicho kimehusisha viongozi mbalimbali wa mkoa wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, ambapo Katibu Tawala alipokea taarifa za maendeleo ya sekta ya kilimo kutoka kila halmashauri. Kupitia taarifa hizo, aliwataka wataalamu wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, umwagiliaji na ardhi kuhakikisha wanatoa usaidizi wa kitaalamu kwa wakulima ili kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Wakuu wa idara ya kilimo kutoka halmashauri mbalimbali walieleza kuwa maandalizi ya kushiriki maonesho hayo yanaendelea vizuri, huku wakulima na vyama vya ushirika (AMCOS) wakishindanishwa ili kupata washiriki bora wenye sifa za kuwakilisha mkoa wa Njombe.
Kwa upande wao, Wakurugenzi wa Halmashauri akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ndg. Jerry Mwaga, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Bi. Kuruthum Sadick, wamesema kuwa sekta ya kilimo inaendelea kupewa kipaumbele kwa kuwa ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya halmashauri, hivyo wanahakikisha inaendelezwa ipasavyo.
Maonesho ya Nanenane hutoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wadau mbalimbali wa kilimo kuonesha teknolojia, ubunifu na mafanikio katika sekta hiyo, sambamba na kupata elimu na maarifa ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.