Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Mh. Deo Sanga amewaagiza viongozi mkoani Njombe kuhakikisha wanamaliza miradi yote viporo iliyoanzishwa na wananchi.
Agizo hilo alilitoa katika kikao cha majumuisho ya kamati ya siasa mkoa wa Njombe,alisema wamegundua kuwepo kwa changamoto katika sekta ya elimu hususani ujenzi wa maboma viporo ya madarasa pamoja na sekta ya afya.
"Vituo vya afya na zahanati havijakamilika,hivyo basi serikali kupitia Halmashauri zote zikamilishe kwa haraka maboma hayo ili wananchi waweze kuhudumiwa kiufasaha"alisema Sanga.
Sanga pia alimuagiza mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka kuunda tume ili kuchunguza miradi miwili mabwawa ya samaki Mtwango pamoja na kituo cha afya cha kijiji cha Ikondo katika halmashauri ya wilaya ya Njombe ambayo haijakamilika huku fedha nyingi ikitumika.
Sanga alisema kamati ya siasa mkoa ilitembelea kata 81 kati ya kata 107 z mkoa wa Njombe na miradi 81 yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 43 pamoja na mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka,alisema kila halmashauri ijipange na kujua idadi ya miradi viporo ili kuikamilisha kwa wakati.
"Tujipange kwamba kwa mwaka wa fedha 2023/24 miradi hii inaenda kumalizika kwa sababu inawahusu wananchi ambao walichangia kwenye mapato yao waliuza mbuzi,kuku na vitu vyengine hilo ni la kitaalamu kwa maana ya CMT na Ras,lakini jengine katibu tawala kukutana na wakuu wa taasisi,meneja wa Tarura,meneja wa Ruwasa,meneja wa Tanesco,meneja wa Tanroad kuangalia kero za msingi"alisema Mtaka.
Naye katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Njombe Josaya Luoga,alitoa onyo baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi wa wilaya za mkoa wa Njombe wanajihusisha na vitendo vya kukihujumu chama hicho kwa kuanza kuandaa wagombea wao watakao gombea nafasi mbalimbali ikiwemo udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2025.
Luoga alisema chama hicho kimebaini uwepo wa viongozi wanaohujumu kazi zinazofanywa na wenyeviti,madiwani na wabunge waliopo madaraka kwa kuwasemea vibaya na kuwanadi watu wao na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu.
"Viongozi hao ni wale wa umoja wa vijana wa chama hicho UVCCM kutoka wilaya ya Ludewa,Makete na Wanging'ombe,tunawajua tunaomba waache mara moja kwa sababu uchaguzi bado"alisema Luoga.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.