Makete, 17 Machi 2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. David Mathayo David, pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), leo imeendelea na ziara yake mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Makete. Katika ziara hiyo, Kamati ilitembelea kijiji cha Mang’oto na kutoa pongezi kwa REA kwa kusimamia mradi huo kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. David Mathayo David, aliipongeza REA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusambaza umeme vijijini. Aidha, aliutaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili maeneo yote yaliyopangwa yaunganishwe kwa wakati. "Tunawapongeza REA kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya umeme vijijini, hususan hapa Mang’oto. Hata hivyo, tunamtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kuhakikisha wananchi wote wanafaidika na huduma hii muhimu," alisema Dkt. Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali inaendelea kutatua changamoto zote za umeme nchini na kuhakikisha vitongoji vyote vinapata nishati ya umeme ili kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi. "Serikali imejipanga kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata huduma ya umeme. Lengo letu ni kuimarisha huduma za afya, elimu na kuwezesha biashara kufanyika usiku na mchana bila vikwazo," alisema Mhe. Kapinga.
Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema serikali inaendelea kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme vijijini, ambapo hivi karibuni wanatarajia kutangaza tenda nyingine ili kuongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi hiyo. "Tunatambua kuwa umeme ni kichocheo muhimu cha maendeleo. Kwa kutambua hilo, tutaongeza juhudi kuhakikisha maeneo yote yaliyobaki yanafikiwa kwa wakati," alisema Mhandisi Olotu.
Wananchi wa Mang’oto wameeleza furaha yao kwa kupata huduma ya umeme kupitia mradi wa REA, wakisema kuwa nishati hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika shughuli za uzalishaji na biashara. Mkazi wa kijiji hicho, Bw. Daniel Mbilinyi, alituma salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi inayowanufaisha wananchi wa vijijini. Katika ziara hiyo, Kamati ya Bunge pia ilifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo, ambapo walipata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu miradi ya umeme na maendeleo kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.