Waziri wa maliasili na utalii Mhe. Pindi Chana,amesema kwa kipindi cha mwezi januari hadi julai mwaka huu jumla ya watalii zaidi ya 4000 walikuja nchini ikilinganishwa na watalii kwa kipindi cha januari hadi julai 2021.
Hatua hiyo imeelezwa jana na waziri huyo wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kutangaza utalii kusini mwa Tanzania uliofanyika mkoani Njombe ambapo alisema ni mafanikio ya mpango wa Royar Tour na kwamba watalii wanaendelea kumiminika.
Akizungumzia changamoto alisema licha ya sekta ya utalii kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi lakini mchango huo hauakisi utajiri wa rasilimali za utalii zilizopo hapa nchini.
Pindi alisema changamoto nyingine inatokana na watalii wengi wanaokuja nchini kutembelea zaidi vivutio vya utalii vilivyopo ukanda wa kaskazini ikiwemo hifadhi za taifa za Kilimanjaro, Serengeti, Ziwa Manyara na eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
Alisema hali hiyo inasababisha siku za watalii ambao wanakuja hapa nchini kukaa kuendelea kuwa chache na watalii kutojirudia.
Alisema katika kufungua utalii kwenye vivutio vya nchi mwaka 2017 serikali ilianzisha mradi wa kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza sekta hiyo katika mikoa ya kusini.
"Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 150 kutoka benki ya dunia" alisema Dk. Chana.
Alisema katika kufanikisha azma ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo mikoa ya kusini wizara ya maliasili na utalii kupitia bodi ya utalii Tanzania imeendaa mikakati mahususi ya kutangaza vivutio vya utalii.
Kaimu mkurugenzi wa bodi ya utalii Tanzania Felix John,alisema utalii ni moja ya sekta za vipaumbele hapa nchini na Rais Samia Suluhu Hassan amejitoa kupitia programu maalum ya Tanzania Royal Tour ili kuitangaza na kuifungua nchi katika sekta ya utalii.
John alisema bodi hiyo imejipanga ili kufungua utalii wa nyanda za juu kusini kwa kuleta watalii kwenye vivutio vilivyopo katika mikoa hiyo.
"Kama mnavyofahamu vipo vivutio vingi katika ukanda huu wa kusini tunayo Kitulo, Mpanga Kipengele na eneo la kihistoria la nyumbanitu" alisema John.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka alisema Tanzania ina hifadhi nyingi na zinafanana lakini upekee uliopo kwa mkoa wa Njombe ni hifadhi ya Kitulo ambayo ni maalum kwa uhifadhi wa maua.
"Kwa maana kama shughuli inafanyika Dar es salaam haya maua inabidi waagize kutoka sehemu nyingine lakini kama ni Njombe yanapatikana hapa hapa" alisema Mtaka.
Alisema watu wengi hawafahamu kuwa hata biashara ya maua inayofanyika mkoa wa Kilimanjaro wilaya ya Moshi na Arusha ilianzia mkoani Njombe.
Alisema biashara hiyo haikufanyika mkoani Njombe kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu ya uwanja wa ndege.
Baadhi ya wabunge wa mkoa wa Njombe wakiwemo Joseph Kamonga na Deo Sanga walisema ili utalii ulete tija kwenye mkoa wa Njombe waliiomba serikali kuharakisha ujenzi wa uwanja wa ndege kwasababu utalii unakwenda sambamba na usafiri wa uhakika.
"Uwanja wetu wa ndege hapa ukamilike ili watalii wawe wanashuka na kuja kwa njia ya ndege na mambo mengine kama kusafirisha parachichi zetu" alisema Sanga.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.