Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ametoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufungua tawi rasmi mkoani humo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima.
Mtaka alitoa kauli hiyo Oktoba 1, 2025, katika kikao maalum cha tathimini ya mbolea kuelekea msimu wa kilimo kilichofanyika ofisini kwake, na kuwahusisha Wakuu wa Wilaya zote za mkoa huo, Maafisa Kilimo, pamoja na wadau wa sekta ya mbolea, ambapo walifanya tathmini ya mahitaji ya mbolea kuelekea msimu mpya wa kilimo.
“Tunahitaji TFRA kuwa karibu zaidi na wakulima wa Njombe. Huu ni mkoa unaotegemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za kiuchumi, hivyo upatikanaji wa pembejeo kwa wakati ni nguzo muhimu ya ustawi wa jamii na maendeleo ya mkoa,” alisema Mtaka.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, aliungana na viongozi hao kujadili changamoto za upatikanaji wa mbolea, ucheleweshwaji wa usambazaji na njia za kuhakikisha pembejeo zinafika kwa wakulima mapema kabla ya msimu kuanza.
Bw. Laurent alibainisha kuwa TFRA iko tayari kushirikiana kwa karibu na Mkoa wa Njombe na kwamba maoni ya viongozi wa mkoa huo yatachukuliwa kama sehemu ya maboresho ya mfumo wa usambazaji wa mbolea nchini.
“Njombe ni miongoni mwa mikoa muhimu katika uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara, na tunatambua haja ya kuwa na uwepo wa kudumu wa TFRA ili kusogeza huduma karibu na wakulima,” alisema Laurent.
Wadau mbalimbali wa kilimo walioshiriki kikao hicho walisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa taarifa za mapema kuhusu upatikanaji wa mbolea, bei elekezi, pamoja na uratibu mzuri baina ya halmashauri na wasambazaji wa pembejeo.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.