Makambako, Oktoba 8, 2025 – Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa, Bi. Subilaga Mwaigwisa, amepokea makabati matano kutoka Mradi wa Imarisha Afya chini ya Shirika la SUMASESU linalofanya kazi katika Wilaya ya Makete na kumilikiwa na Ndg. Ignatio Mtawa. Makabati hayo yatatumika kuhifadhia majalada ya kutolea huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hususan waliothirika na VVU/UKIMWI.
Makabati hayo yamekabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Mji wa Makambako na yanatarajiwa kugawiwa katika kata tano zilizokuwa na uhaba wa vifaa vya aina hiyo. Kata hizo zimebainishwa kuwa na mahitaji makubwa ya miundombinu ya kuhifadhia taarifa muhimu za watoto wanaohitaji uangalizi maalum.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Bi. Mwaigwisa alisema kuwa msaada huo utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za ustawi wa jamii na kuimarisha mfumo jumuishi wa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ngazi ya jamii.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Makambako, Ndg. Masinde Ramadhani, amelishukuru Shirika la SUMASESU kwa msaada huo, akieleza kuwa vifaa hivyo vitaongeza ufanisi na weledi katika utendaji kazi wa maafisa ustawi waliopo kwenye kata husika.
“Msaada huu si tu umetufikia kwa wakati muafaka, bali pia unaenda kuongeza ubora wa huduma tunayotoa kwa watoto wanaohitaji ulinzi na malezi bora kutoka kwa jamii,” alisema Ndg. Masinde.
Msaada huu unadhihirisha ushirikiano mzuri kati ya serikali na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha ustawi wa mtoto unaimarika na huduma zinatolewa kwa ufanisi hadi ngazi ya jamii.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.