Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo, tarehe 19 Februari 2025 alifanya mkutano na wadau wa sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji wa Mkoa wa Njombe katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Jafo alipongeza juhudi za wafanyabiashara wa Njombe katika kukuza uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla. Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji ili kuongeza fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, alipomkaribisha Waziri Jafo, amesisitiza kuwa Njombe ni mkoa wa kimkakati wa kibiashara, ambapo wafanyabiashara wake wanajishughulisha na biashara ndani na nje ya nchi.
"Mkoa wa Njombe ni kitovu cha biashara kinachounganisha masoko ndani na nje ya nchi, ukiwa na wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa na huduma zao kote Tanzania na nje ya mipaka yetu," alisema Mhe. Mtaka.
Aidha, amebainisha kuwa Njombe ni mkoa wenye utajiri wa mazao ya biashara na chakula pamoja na rasilimali za madini na makaa ya mawe, zinazochochea uwekezaji katika sekta ya viwanda.
"Njombe ni mkoa wa kimkakati wa kibiashara, tajiri kwa mazao ya chakula na biashara, rasilimali za madini, na makaa ya mawe yanayochangia maendeleo ya viwanda na uchumi wa Taifa," aliongeza.
Mkutano huo umetoa fursa kwa wadau wa sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji kujadili changamoto na fursa zilizopo ili kuimarisha uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.