Na. Jema Mwanisongole - Njombe
Njombe, Januari 10, 2025 - Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, leo ametembelea kiwanda cha kuchakata mafuta ya parachichi na bidhaa nyingine kinachomilikiwa na kampuni ya Avo Africa Kilichopo Mjini Makambako. Ziara hii ni ishara ya mafanikio makubwa yanayopatikana katika juhudi za kuimarisha uchumi wa mkoa wa Njombe kupitia uwekezaji wa kimkakati.
Kiwanda hicho, ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwezi Februari 2025, ni mradi mkubwa unaolenga kushughulikia changamoto za wakulima wa zao la parachichi, ambalo limekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa mkoa.
"Mwaka 2025 ni mwaka wa suluhisho kwa vilio vya wakulima wa parachichi. Kupitia kiwanda hiki, tunaenda kushuhudia mabadiliko makubwa katika kuongeza thamani ya mazao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi," alisema Mhe. Mtaka.
Uwekezaji huu mkubwa ni sehemu ya juhudi za kutekeleza dira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya uwekezaji nchini. Mheshimiwa Rais Samia amewahi kusema kuwa, “Tunahitaji kuwakaribisha wawekezaji kwa mikono miwili kwa sababu wao ni chachu ya maendeleo na ajira kwa vijana wetu.” Maneno haya yanadhihirika kwa vitendo kupitia kiwanda cha Avo Africa, ambacho kinatarajiwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 400, huku nafasi mpya za ajira zikitarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Mhe. Mtaka alibainisha kuwa mradi huu unaunga mkono jitihada za serikali za kufungua fursa mpya kwa vijana. "Kiwanda hiki siyo tu kwamba kitatoa ajira kwa mamia ya vijana, lakini pia kitapanua wigo wa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla. Ni wakati wa wananchi wa Njombe kufaidika moja kwa moja na fursa hizi."
Avo Africa imewekeza teknolojia ya kisasa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuvutia masoko ya ndani na nje ya nchi. Uwekezaji huu unazidi kuimarisha Njombe kama kitovu cha mazao ya parachichi barani Afrika.
Hii ni hatua kubwa inayodhihirisha kuwa Njombe iko tayari kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kiuchumi kupitia uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.