Njombe, Desemba 25, 2024
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, leo ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kuabudu katika Misa ya Pili iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo hilo, Padre Eusebio Samwel Kyando. Misa hiyo imefanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph na kuhudhuriwa na mamia ya waumini waliojitokeza kusheherekea Siku Kuu ya Krismasi.
Akitoa salamu za Serikali ya Mkoa wa Njombe, Mhe. Mtaka ameeleza kuwa hali ya usalama katika mkoa wa Njombe ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa amani na utulivu. “Mkoa wa Njombe upo salama, na utaendelea kuwa salama wakati wote. Naomba wananchi wote waendelee kusherehekea kwa utulivu na mshikamano,” alisema.
Aidha, Mhe. Mtaka amekemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, hali ambayo imesababisha matukio ya mauaji katika maeneo machache ya mkoa huo. Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaohusika na vitendo vya mauaji au ukatili wa aina yoyote. “Serikali ina mkono mrefu na itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaohusika na ukatili au mauaji. Ni jukumu letu sote kudumisha utu na sheria,” aliongeza.
Pamoja na hayo, amewaasa wazazi na walezi kuendelea kuwajali watoto wao kwa kuhakikisha wanapata lishe bora, akibainisha kuwa Mkoa wa Njombe unaendelea na kampeni kabambe ya kutokomeza udumavu. “Tunaendelea na kampeni ya kutokomeza udumavu hapa Njombe, na ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha watoto wanapata lishe bora ili waweze kukua na kuimarika kiafya,” alisema Mhe. Mtaka.
Tukio hilo limeacha ujumbe mzito wa mshikamano, amani, na umuhimu wa kulinda makundi yote nyeti katika jamii, hususan watoto na wanawake, ili kudumisha maendeleo endelevu.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.