Madiwani wa Njombe Waaswa Kuwa Wahamasishaji wa Maendeleo
Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri za Wilaya ya Wanging’ombe,Makete pamoja na Halmashauri ya Mji wa Makambako wametakiwa kuwa wahamasishaji wa maendeleo na wasimamizi wazuri wa Halmashauri zao, ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kulingana na ahadi walizotoa wakati wa kampeni.
Rai hiyo imetolewa Januari 15, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma S. Sweda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, katika ufunguzi wa mafunzo ya madiwani yaliyofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
“Mmekopeshwa imani na wananchi. Wananchi wana imani na nyinyi kuwa mtaenda kuwa watatuzi wa changamoto, wasimamizi wazuri wa miradi pamoja na kuhamasisha maendeleo kwenye kata zenu. Naamini mtaenda kufanya kazi kwa weledi na utu,” alisema Mhe. Sweda.
Ameongeza kuwa amani na utulivu katika kata zao ni msingi wa maendeleo, hivyo akawataka madiwani kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri katika kuzijenga kiuchumi na kutambua mipaka ya kazi zao.
Mhe. Sweda aliwasisitiza madiwani kuhakikisha wanaongozwa na nyenzo muhimu za utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Dira ya Taifa ya Maendeleo, ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Njombe, Ndg. Lewis Mnyambwa, aliwasihi madiwani kuzingatia ahadi za Serikali katika kutatua changamoto ndani ya siku 100, ikiwemo:Bima ya Afya kwa wote,Ajira kwa Vijana,Uboreshaji wa Miundombinu
Aidha, Ndg. Mnyambwa alibainisha kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa utendaji kazi kwa kuzingatia maadili, uelewa mpana wa kuwahudumia wananchi na kutambua mipaka ya kazi zao.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kwa lengo la kuongeza uelewa mpana kwa madiwani wote wa Halmashauri mkoani Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.