Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amekutana na viongozi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC-TZ) waliofika mkoani humo kwa ziara ya mafunzo ya washiriki wa Kozi ya Kumi na Nne. Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mitaala ya mafunzo ya ulinzi na usalama wa taifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtaka amesema Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa inayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania kutokana na uwepo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na wakazi wake. Ameeleza kuwa mkoa huo una rasilimali muhimu ikiwemo madini yenye thamani kubwa, hususan miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma ya Liganga.
Mtaka amefafanua kuwa Serikali tayari imeshalipa fidia kwa wakazi wa maeneo yanayotekelezwa miradi ya Mchuchuma na Liganga, akibainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni miongoni mwa alama kubwa zitakazokumbukwa katika uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza kuwa miradi hiyo imeingizwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025–2050 na imepewa kipaumbele cha juu miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo Serikali imeelekeza nguvu na rasilimali zake ili kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Brigedia Jenerali PN Songea, amesema ziara hiyo inalenga kuwapatia washiriki uelewa wa vitendo kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na miradi ya Serikali, pamoja na majukumu ya taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kulinda usalama na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Brigedia Jenerali Songea ameeleza kuwa Kozi ya Kumi na Nne inahusisha washiriki 72 kutoka mataifa 17, wakiwemo Watanzania pamoja na washiriki kutoka nchi rafiki. Amebainisha kuwa hali hiyo inaifanya kozi hiyo kuwa jukwaa la kimataifa la kujadili masuala ya ulinzi, diplomasia, usalama na maendeleo.
Katika ziara hiyo mkoani Njombe, washiriki wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna Serikali inavyotekeleza sera zake, pamoja na changamoto na fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.