Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka amewataka wanafunzi na wananchi wa mkoa wa Njombe kwa ujumla kubadili namna ya ulaji wa vyakula ili kuepukana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ulaji mbaya, na ameshauri umuhimu wa kuzingatia lishe bora huku akisisitiza kwamba lishe bora ni kupata mlo kamili na sio kushiba kama ilivyozoeleka kwa jamii nyingi ikiwepo wanafunzi ambao baadaye ndio Taifa la Kesho.
Hayo aliyasema tarehe 17Januari 2024 alipofanya ziara katika shule ya Msingi Nazaleti iliyopo Halmashauri ya Mji Njombe alipokuwa akitoa elimu ya Lishe ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni yenye lengo la kutoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi na namna bora ya ulaji unaozingatia afya.
‘’Lishe bora inaanza na namna ya ulaji kwani lishe bora sio kula na kushiba hivyo ninyi kama taifa la kesho mnapaswa kuzingatia namna ya ulaji bora kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazotokana na ulaji mbaya kwani kumekuwa na wazazi wenye tabia ya kupika vyakula leo chakula hicho kikaliwa na watoto wiki nzima sasa ninyi watoto leo tumewapa elimu hii ya lishe mkawe mabalozi kwa wazazi.amesema Mtaka
Mhe. Anthony Mtaka aliongeza kuwa, watoto wanapaswa kula kwa kuzingatia afya jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za kiafya ikiwa ni pamoja na Ukondefu na Udumavu kwa kutumia vyakula vinavyolinda mwili na kuwataka kuacha mara moja kula vyakula ambavyo vitawasababishia madhara ya kiafya kwa baadaye.
Kampeni ya Lishe Mkoa wa Njombe inaendelea ikiongozwa na Kauli mbiu isemayo, "Lishe ya Mwanao ni Mafanikio yake Njombe tunaweza". Kujaza tumbo si lishe jali unachomlisha.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.