Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amekutana na Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif, kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya afya. Lengo kuu la mazungumzo hayo lilikuwa kuimarisha huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zinazokidhi mahitaji yao.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Mtaka alisisitiza msimamo wake kwa viongozi wa halmashauri kuendelea kutoa ajira za muda mfupi na muda mrefu kwa vijana wenye sifa waliopo ndani ya halmashauri husika. Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza uhaba wa watumishi wa afya na kupunguza tatizo la wasomi waliokosa ajira kurejea katika jamii bila ajira rasmi. Aidha, aliagiza halmashauri zote za Mkoa wa Njombe kuachana na dhana ya kusubiri ajira kutoka Serikali Kuu, akibainisha kuwa kusubiri kumechelewesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi
Kwa upande mwingine, Mhe. Mtaka amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote, akisema mpango huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi waliokuwa hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu. Makundi yatakayonufaika ni pamoja na walemavu, watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wazee pamoja na wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
“Kwa Mkoa wa Njombe zaidi ya kaya 88,000 zinatarajiwa kunufaika na mpango huo, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 12 zitatumika kugharamia huduma za matibabu. Mpango huu ni sehemu ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za afya, na unatarajiwa kutekelezwa ndani ya siku 100 za uongozi wake baada ya kuchaguliwa alisema Mhe. Mtaka”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif, amewataka wahudumu wa kada ya afya katika Mikoa na halmashauri zote nchini kutumia lugha yenye staha na heshima wanapowahudumia wagonjwa. Alisema agizo hilo linatokana na malalamiko ya wananchi kuhusu baadhi ya wahudumu kutumia lugha isiyofaa kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma katika vituo vya afya.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.