MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango,amewataka wadau kujitokeza kuwekeza kwenye miradi ya nishati ya umeme ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa bei nafuu.
Mpango aliyasema hayo wilayani Makete mkoani Njombe,wakati akizindua mradi wa umeme wa ELCT Ijangala Hydropower plant kilowati 360 katika kijiji cha Masisiwe,unaomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kusini Kati wenye thamani ya zaidi ya bilioni tatu.
Dk Mpango alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika ni kichocheo cha maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla.
"Sasa ili tufike hapo,tunahitaji uwekezaji imara na katika uzalishaji, usafirishaji na nishati ya umeme katika maeneo ya uzalishaji na usindikaji wa bidhaa”alisema Dk Mpango.
Aidha Dk Mpango aliligiza Shirika la Umeme nchini Tanesco kulipa fidia wananchi wanaopisha mradi wa umeme wa Rumakali unaotarajiwa kuzalisha megawati 204 katika kijiji cha Madihani Wilayani humo.
Naye naibu waziri wa Nishati Judith Kapinga,alisema wizara itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha vijiji vyote ambavyo havikafikiwa na vinafikiwa.
"Wilaya ya Makete wanakaribia kumaliza kupeleka umeme kwa vijiji vyote 98 tunategemea hadi kufika terehe octoba 30 mwaka huu tutakuwa tumepiga hatua ili Megawati 80 zote za mradi wa Rusumo ziweze kuingia kwenye Gridi ya Taifa"alisema Kapinga.
Kapinga alisema kuwa"Kupitia Rea na Tanesco tunatekeleza miradi mbali mbali ya nishati ikiwemo miradi ya kuzalisha pamoja na kusafirisha umeme sio tu ndani ya nchi yetu lakini Kwa kuunganisha nchi nyingine jirani kama Zambia, Kenya, Uganda, Burundi na Malawi"alisema.
Naye Mkuu wa Dayosisi ya Kusini Kati,Askofu Wilson Sanga alieleza kuwa,ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2021 kama shughuli ya kwanza ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Limited, kampuni iliyoanzishwa na Dayosisi na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Kwa sasa mradi unazalisha umeme wa kilowati 360 na umeunganishwa na Gridi ya Taifa (National Grid) kwa kufuata makubaliano ya kimkataba kati ya TANESCO na Nishati Lutheran (DKK) Investment Limited iliyosainiwa disemba 2020"alisema Sanga.
Meneja wa teknolojia za Nishati vijijini kutoka wakala wa Nishati vijijini (REA)Mhandisi mwandamizi Michael Kessy,alisema REA imetoa takribani milioni 997 kwa awamu tatu tofauti ili kufanikisha mradi huo.
‘’Awamu ya kwanza ilikua katika maandalizi ya mradi ambapo wakala ulisaidia kuandika andiko la mradi pamoja na mpango biashara na pia kuandika andiko la athari za jamii za kimazingira,REA pia ilishiriki katika ujenzi’’alisema Kessy.
Awali mbunge wa Jimbo la Makete Festo Sanga,alimueleza makamu wa Rais changamoto ya ucheleweshwaji wa madai ya fidia kwa wananchi wanaopisha mradi wa umeme wa Rumakali uliopo katika kijiji cha Madihani.
Wakati huo huo Makamu wa Rais,alikabidhi hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe.
Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais,Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda,alisema utolewaji wa hati za hakimiliki za kimila unafuatia uwezeshaji wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji uliofanywa na Wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).
Naye meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Ya Ardhi Pill Msati,alisema ugawaji wa hati hizo unafuatia kazi iliyofanyika na tume hiyo kwa vijiji 64 na kutoa jumla ya hatimiliki za kimila 6,883.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.