Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewahimiza wananchi wa Njombe kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka Novemba 2024.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, wakati wa hitimisho ya ziara ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Mhe. Mtaka alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kuimarisha demokrasia na maendeleo ya mkoa wa Njombe
Mhe. Mtaka alieleza kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni fursa muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi wenye maono ya kuwaletea maendeleo na kusimamia vyema rasilimali za umma. "Wananchi mnapaswa kutumia haki yenu ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huu, ili kuhakikisha mnapata viongozi bora watakaowawakilisha vyema na kuharakisha maendeleo ya maeneo yenu," alisema Mhe. Mtaka.
Aidha, aliwakumbusha wananchi kuwa Serikali za Mitaa zina jukumu kubwa katika kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya, maji, na miundombinu, hivyo ni muhimu kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya. Alisisitiza kuwa kushiriki katika uchaguzi ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa sauti za wananchi zinasikika na maamuzi yanayofanyika yanazingatia maslahi ya wengi.
Mhe. Mtaka pia aliwataka wananchi kuhakikisha wanazingatia amani na utulivu wakati wa kipindi chote cha uchaguzi na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na haki. Alitoa wito kwa vijana, wanawake, na makundi yote ya kijamii kujitokeza kwa wingi, akisema kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuleta mabadiliko endelevu kwa jamii nzima.
Mwisho, Mhe. Mtaka aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia vizuri mchakato wa uchaguzi huo kwa kuhakikisha unafanyika kwa amani, utulivu, na kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za uchaguzi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.