Njombe
Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti Ubora wa Shule, Mwalimu Monica Mpololo, ameongoza ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Mkoa wa Njombe chini ya Mpango wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na mradi wa BOOST. Ukaguzi huo ulihusisha maafisa kutoka OR-TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na wafadhili kutoka Benki ya Dunia.
Lengo kuu la ukaguzi huu ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha mazingira ya utoaji elimu katika shule za msingi na sekondari nchini. Miradi inayokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, madarasa ya awali ya mfano, miundombinu ya elimu, pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ili kuongeza ubora wa elimu nchini.
Wafadhili kutoka Benki ya Dunia walipongeza Mkoa wa Njombe kwa hatua nzuri zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo. Walisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya rasilimali na ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia miradi hii. Aidha, walibainisha kuwa mipango hii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kwenye mazingira bora zaidi.
Mwalimu Monica Mpololo, kwa niaba ya Serikali, aliwahakikishia wadau kuwa jitihada zaidi zinaendelea ili kuboresha elimu, huku akiwataka walimu na maafisa wa elimu kushirikiana kwa karibu kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na manufaa ya wanafunzi wote.
Ugeni huo ulipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, ambaye aliwakaribisha wageni na kupongeza juhudi zinazofanywa kupitia miradi ya SEQUIP na BOOST. Alisisitiza kuwa serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa na kunufaisha wanafunzi wa Njombe.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.