Madiwani Mkoani Njombe wametakiwa kushirikisha wananchi pamoja na wataalamu katika maamuzi yanayofanyika katika kata na halmashauri zao, ili kuepusha migogoro inayosababisha kuchelewesha au kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Imeelezwa kuwa baadhi ya migogoro hiyo hutokana na baadhi ya madiwani kutekeleza majukumu yao kwa kujitenga, bila kushirikiana na wadau wengine muhimu wa maendeleo.
Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo maalumu ya siku tatu kwa madiwani, yaliyowakutanisha madiwani kutoka Halmashauri ya Njombe Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo madiwani kuhusu masuala ya uongozi, utawala bora na namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na ushirikishwaji wa wananchi.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe.Juma Sweda, amesema kuwa migogoro mingi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali na kukwamisha maendeleo inatokana na kutokuwapo kwa maelewano kati ya madiwani na watumishi wa serikali. Amesisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kubadilika mara moja kwa kujenga mshikamano, mawasiliano mazuri na kuheshimiana katika utekelezaji wa majukumu ya kila upande.
“Maendeleo hayawezi kupatikana pale ambapo kuna mgongano wa mawazo kati ya madiwani na watumishi. Kila mmoja ana wajibu wake na wote wanapaswa kushirikiana kwa maslahi ya wananchi,” amesema Sweda.
Kwa upande wao, baadhi ya madiwani wanaoshiriki mafunzo hayo wamesema elimu wanayoipata itakuwa mwarobaini wa kutatua tofauti zilizokuwepo kati yao na wananchi pamoja na watumishi wa serikali. Wameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha mbinu za uongozi na kuimarisha mshikamano.
Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Rozalo Kisumbe kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo), amesema mafunzo wanayoyatoa ni nguzo muhimu ya uongozi bora na wenye tija. Ameeleza kuwa serikali za mitaa ndizo ngazi ya msingi katika kuleta maendeleo ya taifa, hivyo viongozi wake wanapaswa kuwa na uelewa mpana wa majukumu yao na kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na uwazi.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.