TAARIFA YA MGANGA MKUU WA MKOA
KATIKA UZINDUZI WA MKOA WA KAMPENI YA KUPIMA VVU NA KUANZA DAWA MAPEMA, TAREHE 17 JULAI 2018
MKOA WA NJOMBE, VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI ST. BAKITA
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe
Katibu wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Katibu Tawala wa Mkoa,
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya
Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani wote
Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji na Wilaya,
Wajumbe wa Timu ya uendeshaji wa shughuli za Afya Mkoa (RHMT)
Wadau wa Maendeleo katika Mapambano dhidi ya UKIMWI
Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI,
Kikosi kazi kilichobuni na kuandaa kampeni ya Furaha Yangu
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Wanahabari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kuishukuru hadhara hii kwa kuungana nasi katika tukio hili muhimu la uzinduzi wa kampeni hii muhimu ya uhamasishaji wa kupima VVU na kuanza ARV mapema maarufu kama Furaha yangu – Pima, Jitambue, Ishi.
Zaidi ya yote napenda kukushukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na balozi wa kampeni ya Kupima VVU na kuanza ARV mapema maarufu kama Fruha Yangu- Pima Jitambue, Ishi ambayo inaanza kwa kuwalenga wanaume na kisha makundi mengine ambayo ni Wasichana walio katika umri wa balehe, wanawake wenye umri wa miaka 15-24, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao.
Napenda kueleza kwa nini tunawalenga wanaume zaidi katika kampeni hii, pamoja na makundi tajwa hapo juu. Inakadiriwa Kitaifa kuwa asilimia 52.2 ya watu wanaoishi na VVU WANAJUA hali yao ya maambukizi, kiwango hiki ni cha chini sana na hali hii kwa kiasi kikubwa inachangiwa na wanaume ambao kiwango chao cha upimaji kiko chini sana kwa asilimia 45.3 ukilinganisha na kina wanawake ambao ni asilimia 55.9.
Katika Mkoa wa Njombe inakadiriwa kuwa watu 75,000 wanaishi na maambukizi ya VVU na hadi mwisho wa mwezi Machi 2018 watu 48,000 (64%) pekee ndiyo walikuwa wamepima wanapata huduma na tiba katika vituo vya kutolea huduma za Afya, kati yao 16,734 (35%) ni wanaume na 31,266 (65%) ni wanawake.
Ni muhimu sasa kuwahamasisha wanaume kupima VVU na magonjwa mengine na ninawaomba wanawake wawaunge mkono kwa kuwa tayari wameonesha mfano mzuri wa kujali afya zao.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Kampeni ya Furaha Yangu inanipa uthibitisho tosha kuhusu mwitikio wa Serikali ya awamu ya tano katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini, tunamshukuru sana Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake kwa ujumla, Waziri Mkuu na wewe binafsi kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala ya afya ama kwa hakika nyinyi ni Vinara “Machampion” wetu, Tunawaomba muendelee kuwa pamoja nasi katika kuboresha afya za Watanzania.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuupongeza kwa dhati, Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi huu katika Mkoa wetu na kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha kwa waandaaji.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Katika kukabiliana na VVU na UKIMWI nchini toka Mwaka 2015 Serikali imeridhia malengo ya kidunia na tunakusudia kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao, asilimia 90 kati yao wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) na asilimia 90 ya hao wanaotumia ARV kiwango chao cha VVU mwilini kiwe chini/kishuke.
Hali ilivyo Kitaifa kwa mujibu wa takwimu za THIS (Tz HIV Ind. Surney) 2016/2017 ni kwamba kwa;
Tisini ya Kwanza: waliopimwa na kugundulika na maambukizi ya VVU ni asilimia 52.2 ya wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 – 64 ambao wanajua hali zao za maambukizi ya VVU. Wanawake ni asilimia 55.9 na Wanaume ni asilimia 45.3
Kuhusu Tisini ya Pili: Wanaotumia dawa kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 – 64 na ambao wanajua hali zao za maambukizi ni asilimia 90.9, wanawake ni asilimia 92.9. na Wanaume ni asilimia 86.1. kwa takwimu hizi inaonyesha tumepiga hatua nzuri na hata kuvuka lengo kwa ujumla wake kitaifa na kwa kundi la wanawake.
Aidha kwa upande wa Tisini ya Tatu:
Kushuka kwa kiwango cha VVU mwilini, inaonyesha kuwa kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 – 64 na ambao walitoa taarifa kuwa wanatumia ARV ni asilimia 87.7. Wanawake ni asilimia 89.2 na Wanaume ni asilimia 84. Natoa wito kwa wanaotumia ARV kuzingatia masharti na kuwa na ufuasi endelevu wa kutumia ARV.
Hali ya maambukizo ya VVU katika Mkoa wa Njombe:
Kwa mujibu wa takwimu hizo hizo za THIS 2016/2017 kiwango cha maambukizi ya VVU kwa wenye umri wa miaka 15-49 ni asilimia 11.6 kikiwa kiwango cha juu kuliko cha Taifa ambacho ni asilimia 4.7 na kuliko Mikoa yote Nchini Tanzania, kiwango hiki kimeshuka kutoka asilimia 14.8 katika utafiti wa mwaka 2012.
Ndugu Mgeni Rasmi.
Wakati juhudi za kufikia malengo ya 90 mbili za mwisho yanaonyesha mafanikio mazuri, tunaendelea kusuasua kwenye malengo ya 90 ya kwanza inayohusiana na mwamko wa watu kupima na kujua hali zao za maambukizi. Kiwango cha asilimia 52.2 Kitaifa kiko chini sana na hali hii inachangiwa zaidi na wanaume ambao kiwango chao cha upimaji kiko chini sana kwa asilimia 45.3 ukilinganisha na kina mama ambao ni asilimia 55.9. Ndio maana wakati tunasisitiza mwamko wa kupima kwa makundi yote yaliyo katika hatari zaidi ya maambukizi tunatoa wito kwa wanaume na tunakuomba leo uongee na wanaume wote katika Mkoa wa Njombe kushinda uoga na kujitokeza zaidi kupima VVU ili kuchangia mafanikio ya kampeni hii ya Furaha yangu.
Ndugu mgeni rasmi
Kwanini kampeni hii imepewa jina la Furaha yangu – Pima, Jitambue, Ishi?
Kampeni hii tofauti na zilizopita inatoa ujumbe wa furaha kwa wote watakaopima na kujua hali zao za maambikizi. Kwa wale watakaokutwa na VVU sasa wanaanzishiwa matibabu mara moja tofauti na ilivyokuwa zamani walipokuwa wanalazimika kusubiri kuanza dawa mpaka CD4 zishuke au kufikia hatua fulani ya ugonjwa.
Kuanza ARV mapema na kuzitumia kama inavyotakiwa hukata makali ya VVU haraka na kumfanya mtu anayeishi na VVU kuepuka kushuka kwa kinga ya mwili na hivyo kuishi maisha ya kawaida. Hivyo basi, kampeni hii inaleta furaha kwa kumpa mtu maisha marefu ya furaha na amani hata kama ana maambukizi ya VVU.
Sio hiyo tu faraha nyingine ni kuwa iwapo VVU vitaishiwa nguvu, mwenye VVU hataweza kumuambukiza mwenza wake kirahisi. Sasa ni fursa kwa kila mwana Njombe na kila Mtanzania kupima na kuishi kwa furaha bila kujali kama una VVU au huna kwani kwa kutumia ARV una uhakika wa maisha imara.
Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano kupitia ofisi yako kwa kuwezesha uwepo wa vitendanishi na dawa za kutosha kwa wote wanaohitaji huduma hizi.
Nafurahi kukujulisha kuwa katika kipindi hiki cha kampeni huduma za upimaji na kuanzishiwa matibabu zitapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya na katika huduma mkoba hivyo wanachi watapata huduma stahiki.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
Tanzania imekuwa kati ya nchi zinazoonyesha mafanikio katika kupambana na maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa. Tunajivunia kuweza kushusha kiwango cha maambulkizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003 kufikia asilimia 4.7 mwaka 2017/2018 (THIS report).
Haya ni matokeo mazuri ya miaka 30 ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa UKIMWI kupitia kitengo cha kudhibiti UKIMWI (NACP) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na wadau wote Tanzania.
Tuna Imani kubwa kuwa mikakati bunifu ya mabadiliko ya tabia katika kampeni ya furaha yangu itazidi kusaidia kushusha kiwango cha maambukizi ya VVU na hatimae kuutokomeza ugonjwa wa UKIMWI kabisa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
Napenda kuchukua fursa hii pia kuwataarifu watu wanaoishi na VVU na wanaotumia ARV na watanzania wote kwa ujumla kuwa kwa kufuata muongozo mpya wa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na maambukizi ya VVU, hivi sasa tumeanza kutoa ARV kwa wateja wetu kwa miezi mitatu mitatu hasa wale ambao mwenendo wao wa tiba unaridhisha kwa kuwa na kiwango cha VVU mwilini kilichoshuka na wanazingatia umezaji wa ARV na mahudhurio ya Kliniki.
Mpango huu utasaidia kupunguza muda wa walengwa kusubiria huduma vituoni kumuongezea muda wa kufanya shughuli za ujenzi wa Tanzania ya Viwanda kuelekea uchumi wa kati
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Tunawajulisha wote watakao kuwa tayari kupima na kuanza dawa mapema, Serikali na wadau wake kupitia Wizara ya Afya, inafanya ufuatiliaji wa mwenendo wa tiba kwa wanaotumia ARV kwa kupima wingi wa VVU mwilini. Huduma hii sasa itapatikana katika Hospitali yetu ya rufaa ya Mkoa baada ya kupata mashine ya kupima wingi wa VVU mwilini.
Awali tumekuwa tukisafirisha sampuli za vipimo hivyo kwenda Iringa na Mbeya hali iliyokuwa ikizorotesha huduma hii. Pia kwa kushirikiana na wadau wa afya tunaendelea na mpango wa kutumia mashine za Genexpert zinazopima wagonjwa wa TB na kwa kuwa zina uwezo wa kupima Wingi wa Virusi vya UKIMWI zilizowekwa katika Hospital na bahadhi ya vituo vya afya ili kuboresha huduma ya upimaji wa wingi wa VVU.
Pia tumeimarisha upimaji wa CD4 kwa kuweka mashine za CD4 zilizoko katika vituo vya Zahanati na Vituo vya Afya. Pia tumeimarisha upimaji wa Damu (Hb) na Sukari mwilini katika vituo vya afya. Tunaendelea kuhakikisha vitendanishi vya kuwapima maendeleo ya matibabu ya wanaoishi na VVU vinapatikana katika kila wakati.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia ofisi yako inaendelea kutoa Huduma za Tiba na Matunzo kwa wanaoishi na VVU, inakadiriwa kuwa watu wapatao 75,000 wanaishi na VVU katika mkoa wa Njombe, ambapo hadi kufikia Mwezi Machi 2018 watu 48592 waliingizwa katika huduma za tiba na Matunzo na kati ya hao 48,000 wanatumia ARV katika kliniki za tiba na matunzo.
Mpaka Juni, 2018 Mkoa una jumla ya vituo 237 vinavyotoa huduma ya Kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto PMTCT na vituo 62 vinatoa huduma za Tiba na Matunzo.
Hivi sasa Wizara imeanza kutoa ARV kwa watu wote waliopimwa na kugundulika na VVU bila kujali kiwango cha kinga mwili (CD4) na pia tumeanzisha mpango wa kutoa ARV za .miezi miwili kwa watumiaji ambao kiwango cha VVU mwilini mwao kimeshuka.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
Pamoja na mkakati wa kupima na kuanza ARV mapema, Mkoa unaendelea kutumia mikakati mingine kama huduma za tohara kwa wanaume, Matumizi sahihi ya kondomu, Utoaji wa damu salama, mtu kujipima mwenyewe na kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.
Hata hivyo tutatumia njia zote katika mapambano ya UKIMWI lakini bila watu kubadili tabia na mienendo yao hatutaweza kuutokomeza mapema.
Ndio maana napenda kutoa wito kwa mtu mmoja mmoja, makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi na jamii nzima ya Kitanzania kufuta mawazo ya unyanyapaa kwa wenzetu au kujinyanyapaa wenyewe.
Tujitokeze, tukapime, tukikutwa na maambukizi tuanze dawa haraka iwezekanavyo, tutumie dawa kama tulivyoshauriwa, tuwatafute na kuwashauri kwenda kupata huduma ambao tumekuwa na mahusiano ya kingono au watoto waliozaliwa na wanaonyonyeshwa na mama mwenye VVU ili wakapime na kuanza dawa mapema.
Kwa kufanya hivyo sio muda mrefu tutadhibiti ugonjwa huu na tutaiona Njombe bila maambuki na kila mmoja wetu ataiona Furaha yake.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
Mafanikio katika mapambano dhidi ya UKIMWI yanaakisi mafanikio ya nchi katika kutekeleza Lengo Namba Tatu la Maendeleo Endelevu, ninapenda kukuhakikishia kwamba, tunaendelea kutekeleza malengo haya ili ifikapo mwaka 2020 malengo ya Tisini Tatu (90-90-90) yanafikiwa na kuchangia malengo ya kutokomeza UKIMWI duniani ifikapo 2030
Katika kutekeleza mikakati mbalimbali tunaweza kufanikiwa zaidi iwapo kila mmoja wetu atachukua hatua aidha kwa kutumia huduma za afya, kubadili tabia hatarishi, kuacha unyanyapaa na kuchangia Mfuko wa udhamini wa Kudhibiti UKIMWI ambao utaongeza rasilimali fedha pale ambapo Serikali na wadau wameishia. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau ambao baadhi yao ni :-
Serikali ya Marekani kupitia mradi wa USAID Tulonge Afya
Mashirika ya USAID Boresha Afya, Jhpiego SAUTI, Jhpiego AIDS Free
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Viongozi wa dini na vyama vya siasa
Kikosi Kazi cha kampeni hii ya Furaha yangu
Wadu wa habari
Kwa namna ya pekee, ninatoa rai kwa wananchi na wadau wote kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kupima na kuanza ARV mapema.
Nashukuru kwa kunisikiliza.
FURAHA YANGU – PIMA, JITAMBUE, ISHI
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.