SERIKALI kupitia ofisi ya rais Tawala za mikoa na seriakali za mitaa TAMISEMI imekabidhi takribani vitabu 30,355 vya darasa la nne katika Mkoa wa Njombe kwa ajili ya kusaidia kuinua kiwango cha elimu.
Vitabu hivyo vitakabidhiwa kwa Halmashauri nne za Wilaya zilizopo mkoani Njombe,lengo likiwa ni kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa darasa la nne katika shule mbalimbali za mkoani humo.
Akizungumza jana mjini hapa wakati wa kukabidhi vitabu hivyo kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu TAMISEMI, Salum Mkuya alisema utolewaji wa vitabu hivyo na serikali ni mkakati wa kutekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi CCM ili kuinua kiwango cha ufaulu mashuleni.
“Hatuna budi kumpongeza Rais wetu kwa kutekeleza ilani yetu, tumuunge mkono kwa uchapakazi wake mzuri na kuimalisha elimu katika nchi hii, kwa mkoa wa Njombe vitabu ambavyo vimesambazwa ni 30,355,” alisema Mkuya.
“ Katika mgawanyo wa vitabu hivyo ni kwamba Maarifa ya Jamii, 6906, Uraia 6906, Kiswahili 6858, Hisabati 5772, Kingereza 3913,” alisema
Alisema kupitia vitabu hivyo, Halmashauri ya Mji wa Njombe imepokea vitabu 4634.
“Huu ndiyo utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wananchi wake, waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,Madiwani na Wabunge tembeeni kifua mbele,mnapaswa kujivunia, Rais yupo kazini,” alisema Mkuya.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa, Ruth Msafiri aliwataka Walimu mkoani Njombe kuhakikisha vitabu vinatunzwa na vitumike kwa ajili ya kuinua elimu mkoani humo.
“Vitabu hivi vitachochea ufaulu katika mkoa wa Njombe, hususani kwenye Halmashauri ya Mji wa Njombe, ambapo mara zote haijashuka namba mbili kimkoa na inachuana na Halmashauri ya Makambako,” alisema Ruth.
Mtaa wa Lunyanywi
Postal Address: P.O.Box 668-Njombe
Telephone: 026 278 291 213
Mobile:
Email: ras@njombe.go.tz
Copyright ©2019 GWF . All rights reserved.